Wakati mwingine kujilinda waweza kukuita kujitetea,kujiokoa au kujikinga. Ni hali ambapo mtu hufanya jitihada za kujinasua katika tendo ovu ambalo linatekekezwa na mtu mwingine dhidi yake.
Mfano wake ni kama kuvamiwa na majambazi, kutekwa, kufanyiwa fujo ya aina yoyote, kupigwa au kujaribu kupigwa n.k. Matukio ya namna hii au yanayofanana na haya ni sehemu yetu ya maisha. Yumkini yanapotutokea huw tunachukua hatua. Na moja ya hatua ya awali kabisa tunayochukua huwa ni kujaribu kujitetea au kujikinga nayo .
Umevamiwa nyumbani na majambazi, umefanyiwa fujo njiani kwasabasbu yoyote ile na wewe unaamua kujitetea ili usidhurike, na katika kujitetea huko unasababisha kifo cha mtu, awe yule aliyetaka kufanya fujo au mwingine mpita njia. Sheria inasemaje kuhusu mkasa wa aina hii. Makala yataeleza japo mambo ya msingi kuhusu hali hii.
1.HAKI YA KUJILINDA.
Haki ya kujilinda ni haki ya kisheria. Ni haki ambayo ipo kwa kila mtu. Mbali na kuwa haki hii ni ya kisheria pia haki hii ni ya kuzaliwa. Kuna tofauti kati ya haki kuwa kisheria na kuwa ya kuzaliwa.
Haki za kisheria ni zile haki zote ambazo zimeelezwa ndani ya sheria. Zimekuwepo baada ya sheria kutungwa na hivyo kabla ya sheria kutungwa hazikuwepo. Haki ya kuzaliwa ni haki ambayo imekuwepo tangu mwanadamu wa kwanza alipokuwepo. Ni haki ambayo mtu anazaliwa nayo.
Haki hii haihitaji kuwa ndani ya sheria ili mtu awe nayo isipokuwa tu anapozaliwa nayo huzaliwa. Hukua nayo na hufa nayo. Kujilinda au kujitetea pale mtu anapotaka kukudhulu hakuihitaji kuwa ndani ya sheria ili ndo umzuie asikudhulu. Isipokuwa ni jambo ambalo hutokea lenyewe(automatic).Lipo tu hata sheria isiliseme.
Kwahiyo pamoja na kuwa haki ya kujilinda usidhurike ni haki ya kisheria lakini kubwa zaidi ni kuwa haki hii ni haki ya kuzaliwa.
Haki nyingine za kuzaliwa ni kama haki ya kuishi, ukishazaliwa haki ya kuishi inakuwepo sio mpaka iwe kwenye sheria, haki ya kuzungumza, ikiwa umezaliwa unazungumza basi hiyo ni haki ambayo husubiri sheria iitoe, haki ya kutembea n.k. Haki ambazo si za kuzaliwa ni kama hizo za kuchagua au kuchaguliwa, kupiga kura, haki elimu n.k.
2. UNAPOSABABISHA KIFO UKIJARIBU KUJILINDA/KUJITETEA.
Kifungu cha 18 cha Kanuni za adhabu , sura ya 16 kinasema kuwa mtu hawezi kuwajibika kijinai kwa kitendo alichokifanya wakati wa kutimiza haki yake ya kujitetea, kumtetea mtu mwingine, au kutetea mali.
Kifungu hiki kinasomwa na kifungu cha 18c kinachosema kuwa haki ya kujilinda, kumlinda mtu mwingine au mali itatumika kwa mtu yeyote ambaye katika kutumia haki hiyo atasababisha kifo au dhara kubwa kwa mtu mwingine.
Maana ya vifungu hivi ni kuwa haki ya kujilinda itatumika kama kinga kukuondolea hatia ya jinai iwapo umesababisha kifo. Lakini ili ikubalike kama kinga na usitiwe hatiani kwa kosa la kuua vifungu hivi vimetoa masharti yafuatayo.
( a ) Kwanza wewe uliyesababisha kifo uwe umesababisha kifo hicho kwa nia njema kwa maana ya kuwa ulikuwa kweli kabisa ukijilinda usidhulike. Isije kuwa unatumia nafasi ya kujilinda kumuua au kumdhulu mtu mwingine kwa makusudi ukijifanya ulikuwa ukijilinda. Swali la ulifanya makusudi au kwa nia njema ya kujilinda litathibitishwa kitaalam na mazingira ya tukio husika.
( b ) Kitendo ulichofanyiwa kiwe ni kitendo ambacho kiukweli ulitakiwa kutumia nguvu kiasi cha kusababisha kifo. Isiwe mnatupiana maneno mawili matatu halafu unasababisha kifo kwa kisingizio kuwa ulikuwa ukijilinda usidhulike. Kuwe na mazingira ambayo hata ukiyatizama yafanane na hatua ya kujikinga hadi kusababisha kifo.
( c ) Pia ikiwa kitendo kinahusu kubaka au kufanya kinyume na maumbile kinga ya kujikinga hadi kusababisha kifo inaswihi.
( d ) Pia kujikinga/kujitetea hadi kusababisha kifo kunakubalika ikiwa tendo linahusisha kuteka nyara, au kutorosha.
( e ) Pia matendo kama kuvunja na kuingia, unyanganyi, kuchoma moto, nayo yanakubalika katika kujikinga hadi kusababisha kifo.
Kwa kumalizia zingatieni kuwa ikiwa upo katika mazingira ambayo unaweza kujikinga/kujitetea bila kusababisha kifo au madhara makubwa basi ni vema kufanya hivyo. Kujikinga hadi kuua liwe chaguo la mwisho pale unapokuwa huna namna nyingine yoyote isipokuwa kufanya hivyo.
You may contact us through
Email : lawyersheria@gmail.com
phone number: +255 620 212 960