Yapo mambo unayotakiwa kufanya mara tu baada ya kusajili kampuni. Tunazungumzia yale utakayoyafanya ule mda baada ya kuwa umepewa cheti cha kuzaliwa kwa kampuni( certificate of incorporation) kutoka BRELA. Mambo haya ni ya kisheria na kutoyafanya kwake kunahesabika ni kuvunja sheria.
Kwahiyo mambo haya ni lazima na sio hiari.
Hata hivyo kabla ya kueleza hayo ni muhimu tukajikumbusha kuhusu taratibu za kusajili kampuni. Tunasema kujikumbusha kwakuwa makala kuhusu taratibu nanamna ya kusajili/kuunda kampuni hatua kwa hatua yalishaandikwa hapo awali.
Haya yote yatakuwa yakitoka Sheria ya Makampuni ,Namba 12 ya mwaka 2002.
1.HATUA ZA KUSAJILI/KUUNDA KAMPUNI.
( a ) Kwanza hakikisha unajua unahitaji kufanya biashara gani. Hii ni kwasababu katika vitabu vya kampuni lazima uandike biashara unayotaka kufanya au unayofanya tayari.
( b ) Hakikisha mko wawili au zaidi. Hakuna kampuni ya mtu mmoja. Kampuni binafsi huanzia watu wawili na mwisho ni watu 50. Unaweza kuwa wewe na mke wako, rafiki, ndugu, mzazi, mtoto nk.
( c ) Fahamu kampuni yenu inatakiwa kuwa na hisa ngapi na kila hisa itakuwa inauzwa bei gani. Pia unatakiwa kujua kampuni itakuwa na mtaji wa shilingi ngapi. Kwa mfano kampuni itakuwa na hisa 10000, bei ya kila hisa ni Tshs 1000 ambapo, hisa x bei ya hisa = mtaji wa kampuni, kwa maana ya 10000 x 1000 = 10000000 ambao ndio mtaji wa kampuni.
( d ) Andaa jina ambalo ungependa kampuni yako iitwe. Jina lolote linakubalika isipokuwa lisiwe tayari linatumiwa na kampuni nyingine au lisiwe kwa namna moja au nyingine lina viashiria vya matusi au lugha isiyostahiki.
( e ) Peleka maombi BRELA kuhusu jina ulilochagua kwa uhakiki. Uhakiki wanaangalia kama linatumiwa na kampuni nyingine tayari au linavyo viashiria vya lugha isiyostahiki. Siku hizi uhakiki hufanyika kupitia mtandao( online search/name clearance).
( f ) Baada ya kuwa jina limepitishwa basi utatakiwa kuandaa waraka na katiba ya kampuni( memorundum & article of association) ikiwa ni pamoja na kujaza fomu ambavyo kwa pamoja vitapelekwa BRELA kwa usajili.
2. BAADA YA KUSAJILI FANYA HAYA.
( a ) Hakikisha unapata namba ya mlipa kodi pamoja na leseni ya biashara kabla hujaanza kufanya biashara.
( b ) Kama kampuni yako ni binafsi ( private limited) hakikisha nyaraka zote za kampuni kama barua, mikataba , bango la nje nk. unaweka neno LIMITED baada ya jina la kampuni, mfano KIKWE COMPANY LIMITED. Na kama ni ya umma( public limited) andika neno PLC ( Public Limited Company) baada ya jina. Kutoweka neno limited au PLC ni kosa kwa mujibu kifungu cha 34 cha sheria ya Makampuni.
( c ) Hakikisha unaweka bango lenye jina la kampuni nje ya ofisi. Kifungu cha 112 cha Sheria ya Makampuni kimeweka ulazima katika hilo.
( d ) Hakikisha kila mwaka kampuni inafanya mkutano mmoja wa jumla( annual general meeting). Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 133 cha Sheria ya Makampuni. Mkutano huu ni wa lazima.
( e ) Kujaza fomu ya hisa kwa kila aliyechukua hisa za kampuni ndani ya siku 60. Hili linakwenda sambamba na kutoa cheti cha umiliki wa hisa ( share certificate) kwa kila aliyechukua hisa na kuzilipia.
( f ) Mwisho hakikisha unafanya mrejesho wa kila mwaka ( annual return) kwa mujibu wa kifungu cha 128 cha Sheria ya Makampuni. Hii ni fomu maalum ambayo hujazwa na kupelekwa BRELA kila mwaka. Hueleza hali ya kampuni ikoje kwa mwaka mzima hasa kuhusu ofisi ilipo , wanahisa, hisa, wakurugenzi, nk.
Post a Comment