Kwa mujibu wa sheria ya usajili wa ardhi sura ya 334 ipo aina ya mikataba ya pango ambayo baada ya kuwa imeingiwa kati ya mpangaji na mwenye nyumba/eneo ni lazima isajiliwe. Mikataba ya aina hiyo isiposajiliwa inakuwa haijakidhi vigezo vya kisheria na hivyo kubatilika.
Aidha pango huhusisha shughuli mbalimbali. Yapo mapango kwa ajili ya biashara maduka, bar, mahoteli n.k. na pia yapo mapango kwa ajili ya makazi. Iwe umepanga kwa ajili ya biashara au makazi madhali aina yako ya upangaji inahitaji kusajiliwa kisheria basi huna budi kufanya hivyo ili uhalali wa pango lako upatikane.
Kabla ya kuona aina ya mikataba ya pango ambayo ni lazima kusajiliwa ni vyema kujikumbusha kidogo kuhusu haki za mpangaji.
1.HAKI ZA MPANGAJI.
( a ) Haki ya kutoingiliwa na mwenye nyumba ili kumpa uhuru mpangaji kufurahia pango lake.
( b ) Haki ya kumpa taarifa(notice) mapema mpangaji ikiwa mwenye nyumba anataka kukagua nyumba/eneo lake.
( c ) Haki ya kutoondolewa au kusitishiwa mkataba mpaka baada ya kupewa taarifa maalum( notice) .
( d ) Haki ya kuambiwa ukweli kuhusu hali ya nyumba kabla ya kusaini mkataba wa pango. Mfano kuambiwa ikiwa eneo linajaa maji kipindi cha mvua, kuambiwa ikiwa nyumba inavuja n.k.
( e ) Haki ya kukataa sharti lolote ambalo linalenga kuminya uhuru wa mpangaji au linalovunja sheria yoyote ya Tanzania.
( f ) Haki ya kupewa taarifa mapema(notice) kabla ya kupandisha kodi ya pango.
( g ) Haki ya kupewa taarifa mapema(notice) kabla ya kubadilisha sharti lolote katika mkataba wa pango.
Haki ni nyingi hizi ni baadhi tu.
2. MKATABA WA PANGO AMBAO NI LAZIMA KUSAJILIWA.
Kifungu cha 54 ( 1 ) cha Sheria ya Usajili wa Ardhi , Sura ya 334 kinasema kuwa pango ambalo mkataba wake unazidi miaka mitano linatakiwa kusajiliwa.
Wapo watu wanapanga mahoteli, bar, maduka nk. ambao miaka ya pango katika makubaliano yao ni zaidi ya mitano. Hawa mikataba yao ni lazima isajiliwe.
Mara nyingi mkataba wa pango huweza kuwa wa miaka mingi kutokana na aina ya biashara anayotaka kufanya mpangaji halikadhalika uwekezaji anaotarajia kufanya eneo analotegemea kupanga. Wakati mwingine mpangaji hukubaliana na mwenye eneo kufanya marekebisho makubwa ( renovation) ili enepo lifanane na aina ya biashara anayotaka kufanya.
Mbali na hayo ni vema kufahamu pia kuwa mkataba ambao ni chini ya miaka mitano lakini mkataba huo una sharti la kuhuisha( renew) kwa miaka mingine, ambapo ukijumlisha miaka ya awali na hiyo ya kurenew jumla inazidi mitano basi nayo ni lazima kusajiliwa.
Tumeongelea mikataba inayozidi mikaka mitano lakini hatupaswi kusahau kuwa hata mikataba ya pango iliyo chini ya miaka mitano inaweza kusajiliwa japo sio lazima. Mikataba hii una chaguo kusajili au kutosajili. Kisheria kutosajiliwa kwake kwa namna yoyote hakuathiri uhalali wake.
4. WAPI UKASAJILI.
Msajili wa nyaraka anayepatikana ofisi za ardhi ndiye anayehusika na usajili wa mikataba hii. Unapofika ofisi yoyote ya ardhi utapewa maelekezo lipi la kufanya ili mkataba wako uweze kusajiliwa.
Aidha ipo ada ya kulipa kabla ya usajili ikiwemo kodi ya faida.
Post a Comment